Licha ya kikosi chake kuonekana kuimarika, Kocha Mkuu wa Simba Fadlu Davids bado amehitaji maboresho zaidi katika usajili wa dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa Disemba 16 hadi Januari 15 2025
Baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa watani zao Yanga katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa Oktoba 19, Fadlu alidokeza kuwa lazima yafanyike maboresho katika baadhi ya maeneo ili kuwa na timu imara zaidi
Imeelezwa kuwa kocha huyo amehitaji wachezaji watatu ambao anaamini wataongeza ubora katika maeneo yenye changamoto
Tayari Simba imemsajili winga Elie Mpanzu kutoka klabu ya AS Vita ambapo mchezaji huyo anasubiri kufunguliwa kwa dirisha dogo
Mpanzu yuko nchini akiendelea kujifua na kikosi cha Simba kinachofanya mazoezi yake katika uwanja wa Mo Simba Arena
Kiungo mshambuliaji Foday Trawally raia wa Gambia, anayekipiga Klabu ya Cetinkaya TSK ya Uturuki ni jina la pili linalotajwa kuelekea Msimbazi
Simba ilifanya jitihada za kumsajili nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 katika dirisha lililopita la usajili lakini haikuwezekana
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya klabu hiyo, zinasema mazungumzo baina ya pande mbili yameshaanza na Simba inataka kumpa mkataba wa miaka mitatu mchezaji huyo
Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kinasema kuwa Simba imeamua kuongeza kiungo mshambuliaji anayechezea klabu hiyo iliyopo Ligi Draaja la Pili nchini humo, ili kuwasaidia wachezaji wawili kwenye eneo hilo ambao ni Jean Charles Ahoua na Awesu Awesu
"Ni usajili unaotokana na matakwa ya kocha, amesema anahitaji dirisha dogo waingie wachezaji watatu wa viwango vya juu vya kimataifa kwa ajili ya mechi kubwa:
"Mchezaji huyu ni kiungo mshambiliaji, ambaye kazi yake itakuwa ni kusimama nyuma ya washambuliaji, kutengeneza nafasi na kutoa pasi za mwisho"
"Skauti yetu imejiridhisha kuwa ni mchezaji bora na anayefaa kwa kazi hiyo, kocha anahitaji kiungo anayetengeneza nafasi rahisi zaidi kwa mastraika na huyu ndiye chagua," kilisema chanzo hicho
Mbali na mchezaji huyo, habari zinasema Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, anahitaji beki wa kati ambaye ni mrefu na mwenye nguvu kwa ajili ya michezo migumu ya kimataifa kwani anadai mabeki wake tegemeo ni wafupi, hivyo anayekuja anaweza kumsaidia kwa kiasi kikubwa kutengeneza ukuta imara zaidi