Baada ya mchezo dhidi ya JKT Tanzania kuahirishwa, Wekundu wa Msimbazi, Simba Sc wameweka nguvu katika mchezo unaofuata dhidi ya Mashujaa Fc ambao utapigwa Ijumaa, Novemba 1 katika uwanja wa Lake Tanganyika
Kikosi cha Simba jana kilionekana kikifanya mazoezi katika mchana wa jua kali, ikielezwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Fadlu Davids anawaandaa vijana wake kukabiliana na mazingira ya joto kali mkoani Kigoma hasa ikizingatiwa mchezo huo utapigwa saa 10 jioni
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ali amesema timu inaandaliwa vyema ili kuhakikisha wanabeba alama zote tatu Kigoma
"Tupo kwenye maandalizi makali, na tunafanya maandalizi ya safari ili kuelekea mjini Kigoma kucheza na Mashujaa, kwa hiyo nawaambia wanachama na mashabiki wote wa Simba, baada ya kuahirishwa mchezo wetu dhidi ya JKT Tanzania, nguvu zote sasa tunaelekeza Kigoma dhidi ya Mashujaa Novemba Mosi"
"Furaha yetu imesogezwa mbele, tukutane Kigoma tukafurahi tena," alisema Ahmed
Simba imeshinda mechi zote ilizocheza ugenini msimu huu, alama tano walizopoteza ni katika mechi ambazo walikuwa nyumbani
Wekundu hao wa Msimbazi wanashika nafas ya tatu katika msimamo wa ligi wakiwa na alama 19