Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo ambapo mchezo mmoja unapigwa mkoani Kigoma. Mashujaa Fc watakuwa wenyeji wa Simba katika mchezo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini
Wekundu wa Msimbazi waliotua Kigoma jana, watashuka dimba la Late Tanganyika wakifahamu ushindi dhidi ya Mashujaa leo utawahakikishia kusogea nafasi ya pili katika msimamo wa ligi
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo na malengo yao ni kupata pointi tatu ili kujiimarisha katika msimamo wa ligi hiyo
Fadlu amesema anatarajia mechi hiyo itakuwa ngumu lakini wachezaji wake wamejipanga kuonyesha kiwango cha juu baada ya kupata mapumziko tofauti na walivyokuwa katika michezo iliyotangulia
Naye Kocha Msaidizi wa Mashujaa, Maulid Makata, amekiri mchezo utakuwa mgumu kwa sababu wanakutana na timu kubwa lakini msimu huu ikiwa bora zaidi kuliko msimu uliopita
Makata amesema hata hivyo wachezaji wake wanapenda kucheza mechi za aina hiyo ambazo zinawatazamaji wengi uwanjani na katika televisheni
"Mechi kama hizi makocha kazi yetu ni kuwajenga tu kisaikolojia kwa sababu wachezaji wenyewe wanazitaka, wanajua zinaonekana na watu wengi kwa hiyo nao wanataka waonekane, wajiuze"
"Tunajua wenzetu ni timu kubwa na wana maandalizi makubwa kuliko sisi, huwezi kutulinganisha na sisi, ukiangalia malengo yao ni kutwaa ubingwa na sisi kubaki Ligi Kuu au nafasi ya nne, ila katika mpira chochote kinaweza kutokea," alisema kocha huyo