Mabingwa watetezi Ligi Kuu ya NBC Yanga leo wako dimbani Azam Complex kuikabili Tabora United katika mchezo utakaopigwa saa 12 jioni
Yanga inakwenda katika mchezo huo bila ya walinzi wake tegemeo Ibrahim Bacca na Dickson Job wanaotumikia adhabu
Bacca alionyeshwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Azam Fc ambapo atakosa mechi tatu huku Job akitumikia adhabu ya kadi tatu za njano
Yanga pia huenda wakakosa huduma ya mlinzi wa kulia Yao Kouassi, mkufunzi wa Yanga Miguel Gamondi akithibitisha bado hajapona majeraha aliyopata katika mchezo dhidi ya Coastal Union
Ni mchezo unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali, Tabora United wako katika kiwango bora wakishinda mechi mbili zilizopita dhidi ya Mashujaa na Pamba Jiji
Aidha huenda leo nyota wa zamani wa Yanga, washambuliaji Heritier Makambo na Yacouba Songne wakaongoza safu ya ushambuliaji ya Tabora United dhidi ya waajiri zao hao wa zamani
Yanga wako nafasi ya pili katika msimamo wa ligi wakiwa na alama 24, nyuma ya watani zao Simba wanaoongoza ligi baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya KMC jana na kufikisha alama 25
Kama Yanga itaibuka na ushindi leo basi itarejea juu ya msimamo huku Tabora United wakiwa nafasi ya sita na alama 14