Baada ya kuwa nje ya uwanja wa takribani mwaka mzima, kiungo wa Azam Fc Sospeter Bajana amesema ana kazi ya kufanya ili kuhakikisha anarejea katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo
Eneo la kiungo la Azam Fc inayoshika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kwa sasa linamilikiwa na viungo James Akaminko na Adolf Mtasingwa huku Feisal Salum 'Fe Toto' akitumika kama kiungo mshambuliaji
Bajana amekiri sio rahisi kurudi moja kwa moja kikosini kutokana na uwepo wa wachezaji hao ambao wanafanya vizuri hivyo analazimika kupambana katika uwanja wa mazoezi
"Nilikuwa nje ya uwanja ni mwaka sasa siwezi nikarwejea moja kwa moja kucheza wakati kuna wachezaji wanafanya vizuri na wanaipambania timu kufikia malengo nina kazi ya kufanya kuhakikisha namshawishi kocha aniamini na kunipa nafasi"
"Naheshimu ubora wa Adolf Mtasingwa na James Akaminko ambao wamekuwa wakicheza nafasi ambayo na mimi naicheza kila mmoja anafanya majukumu yake kwa ubora nafikiri ili kuweza kucheza natakiwa kufanya kazi ya ziada" alisema
Kocha wa Azam Fc Rachid Taoussi amesema wachezaji wengi eneo moja na wote wakiwa bora ni chachu ya mafanikio kwake kutokana na wingi wa mechi na ratiba ngumu ya mechi mfululizo itamsaidia kufanya mabadiliko ya mara kwa mara
"Kuna mechi nyingi nafurahia wachezaji wengi wamerudi na wengine wanarudi kidogo kidogo naamini wote wakiwa kwenye ubora unaotakiwa tutakuwa na timu ambayo inaonyesha ushindani kwa wapinzani bila kuchoka kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara eneo hilo la kiungo"
"Bajana bado hajawa fiti lakini tayari ameanza mazoezi ni mchezaji mzuri ataongeza kitu hasa ushindani katika eneo la kiungo mkabaji ambalo tayari wachezaji waliopo wameonyesha uwezo mkubwa," alisema