Stars kuifuata Ethiopia Alhamisi

Joel JJ By Joel JJ β€’ 13th November 2024


Stars kuifuata Ethiopia Alhamisi

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inatarajia kuondoka nchini kesho Alhamisi kwa ajili ya mchezo wa tano wa kusaka tiketi ya kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, dhidi ya Ethiopia, mechi itakayopigwa Jumamosi

Stars inaingia katika mchezo huo wa tano wa kundi 'H' ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa suluhu mechi ya mwisho dhidi ya Ethiopia iliyopigwa Septemba 4, mwaka huu, huku kwa upande wa Wahabeshi hao wakipoteza kwa mabao 3-0, mbele ya Guinea

Akizungumzia maandalizi kwa ujumla, kaimu kocha mkuu wa Stars, Hemed Suleimani 'Morocco' alisema, licha ya ugumu wa mchezo huo ila wao kama benchi la ufundi na wachezaji kiujumla wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo chanya ugenini

"Kila mmoja wetu yupo tayari kwa changamoto nyingine, tunatambua wapinzani wetu wamekuwa na matokeo yasiyoridhisha sana ila tutacheza kwa tahadhari ya kuhakikisha tunashinda, mchezo huu utatoa taswira yetu ya kufuzu AFCON mwakani Morocco"

"Wenzetu DR Congo walishafuzu hivyo presha ipo kwetu na Guinea ambayo iko juu yetu kwenye msimamo, mchezo na Ethiopia tunauangalia kwa jicho la tatu kwa sababu ndio utakaotupa matumaini makubwa kuelekea mechi ya mwisho hapa Dar es Salaam,"  alisema Morocco

Stars itacheza mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa des Martyrs huko Congo na baada ya hapo itacheza na Guinea jijini Dar es Salaam Novemba 19


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.