Morocco aahidi ushindi dhidi ya Ethiopia leo

Joel JJ By Joel JJ β€’ 16th November 2024


Morocco aahidi ushindi dhidi ya Ethiopia leo

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kiko ugenini huko DR Congo kuchuana na wenyeji Ethiopia katika mechi ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Des Martyrs, Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo)

Mechi hiyo itachezwa kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania na Ethiopia imeamua kucheza mechi zake Kinshasa kwa sababu ya kutokuwa na viwanja venye hadhi ya kutumiwa katika michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)

Stars inahitaji pointi tatu muhimu leo na pia kuifunga Guinea katika mechi ya mwisho ya Kundi H itakayofanyika Novemba 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam

Kocha Mkuu wa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco', amesema amewaandaa vijana wake kwa ajili ya kusaka ushindi

"Maandalizi yameshakamilika, nimejaribu kuwaelekeza vijana wangu nini cha kufanya na kupunguza madhaifu yote yaliyoonekana katika michezo iliyotangulia, niseme tuko vizuri na lengo letu ni kupata pointi tatu ambazo zitatusogeza kwenye mlango wa kuingilia kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON)," alisema kocha huyo

Mbwana Samatta, ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa, amesema yeye na wachezaji wenzake wote wanaelewa umuhimu wa mchezo wa leo, hivyo watajitoa kupambana ili kupata ushindi kwa sababu endapo watashinda katika mchezo huo watajiweka kwenye wakati mzuri zaidi

"Kila mchezaji anafahamu umuhimu wa mchezo huu na unaofuata, sidhani kama kuna muda wa kukumbushana tena. Mwalimu ameshamaliza kazi yake, ametupa mbinu na mipango, ni jukumu letu sasa kuonesha uwanjani. DR Congo wameshafuzu, tunagombea nafasi moja, sisi (Tanzania) na Guinea ndiyo tunapewa nafasi kubwa, hivyo tunataka tuitumie nafasi hiyo," alisema Samatta

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Septemba 4, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana

Stars yenye pointi nne ipo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo nyuma ya Guinea yenye pointi sita huku Ethiopia inaburuza mkia kiwa na pointi moja. Mechi nyingine ya kundi hilo itachezwa leo kati ya Guinea dhidi ya DR Congo ambayo tayari ina pointi 12 kibindoni.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.