Baada ya wiki mbili za mapumziko ya kalenda ya FIFA, Ligi Kuu ya NBC inarejea kesho Ijumaa ambapo mchezo mmoja kati ya Pamba Jiji dhidi ya Simba utapigwa uwanja wa CCM Kirumba
Wakizungumza katika Mkutano na Wanahabari mapema leo, makocha wa timu hizo Fred Felix Minziro (Pamba Jiji) na Fadlu Davids (Simba) wametamba timu zao kupata matokeo mazuri katika mchezo huo
Kocha Mkuu wa Simba Fadlu amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo wakiwa na malengo ya kuondoka na alama zote tatu
Licha ya ratiba ya mchezo huo kuwa ni siku chache baada ya mechi za Kimataifa katika kalenda ya FIFA, Fadlu amesema hakuna athari zozote katika maandalizi kwani wachezaji wake waliokuwa timu za Taifa, wametumika
"Tuko hapa Mwanza wachezaji wakiwa na ari na morali kubwa kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Pamba Jiji. Tumekuwa na maandalizi mazuri kuelekea mchezo huu"
"Ratiba ya mechi za kalenda ya FIFA haijatuathiri kwa sababu wachezaji wengi wametumika katika timu zao za Taifa"
"Wachezaji wako timamu kimwili na kiakili kuelekea mchezo dhidi ya Pamba Jiji hapo kesho," alisema Fadlu
Nae Minziro ambaye aliingoza Pamba Jiji kupata ushindi wa kwanza msimu huu kwa kuichapa Fountain Gate mabao 3-1 kabla ya mapumziko ya kalenda ya FIFA, amesema amepata muda mzuri wa kufanya maandalizi hivyo wakazi wa Mwanza watarajie timu yao kupata matokeo mazuri katika mchezo dhidi ya Simba
"Nimefurahi, nimepata muda wa kutosha wa kufanya maandalizi, kuwasoma wachezaji wangu na kufanya marekebisho muhimu. Niseme tu kesho mashabiki wetu watarajie kupata burudani,"alisema Minziro
Simba iko kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imekusanya alama 25 kutoka mechi 10 wakati Pamba Jiji wanashika nafasi ya 15 wakiwa na alama 8



