Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema hatafanya mazoezi yoyote ya mbinu wakiwa Algeria ili kutowapa nafasi wapinzani wao, CS Constantine kufahamu mfumo watakoutumia
Jumapili, Disemba 08 Simba itawavaa wenyeji CS Constantine katika mechi ya Kundi A ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC)
Muda mfupi kabla ya Simba kuondoka Tanzania jana, Fadlu aliweka bayana kuwa aina ya mazoezi watakayofanya Algeria ni kuwaweka fiti kimwili wachezaji wake kwa kuchezea mpira tu
Fadlu alisema maandalizi yote muhimu ya mchezo huo yalimalizikia wakiwa Tanzania, kinachofanyika ugenini ni kuondoa uchovu wa safari
"Tutakachokifanya ni kuhakikisha wanakuwa sawa upande wa utimamu wa mwili tu, kwa sababu ni hatari kufanya mazoezi ya mbinu ya mchezo huo kwa sasa"
"Tulimaliza mazoezi ya kimbinu pamoja na kuyafanyia kazi mapungufu na ubora wa wapinzani wetu tukiwa Tanzania. Huku yatakuwa ni mazoezi ya kawaida tu ya kuweka miili sawa kwa sababu macho yatakuwa mengi kututazama, siwezi kufanya mazoezi ya kimbinu au chochote kile kinatachowafanya wapinzani wetu hata kuhisi tunacheza vipi," alisema
Fadlu amesema anatarajia itakuwa mechi ngumu hivyo amewaandaa wachezaji wake vyema hasa eneo la kujilinda na hatari za wapinzani wao katika mechi hiyo ya kwanza ugenini
"Tunatakiwa tuwe vizuri zaidi katika eneo la kuzuia huku tukijiepusha kufanya makosa mengi. Tumefanya mazoezi ya kuimarisha safu ya ulinzi na nafasi ya kiungo wa kukaba kwa sababu tunacheza ugenini, pia tunatakiwa kushambulia kwa haraka tukiwa na mpira na kurudi mapema," aliongeza Fadlu
Simba na CS Constantine zilishinda mechi zao ya raundi ya kwanza kwa ushindi wa bao 1-0 hivyo mchezo huo unaweza kuamua timu itakayokaa kileleni
Matokeo ya ushindi yatakuwa matokeo bora zaidi kwa Simba ugenini lakini hata matokeo ya sare yataiweka Simba katika nafasi nzuri ya kukamilisha malengo yake ya kuzufu robo fainali