Klabu ya Simba imerejea nchini Alfajiri ya leo Jumanne wakitokea Algeria katika mchezo wa raundi ya pili hatua ya makundi kombe la Shirikisho dhidi ya CS Constantine ambao walipoteza kwa kufungwa mabao 2-1
Wakati Simba ikitua, wapinzani wao katika kundi A, CS Sfaxien ya Tunisia nayo imetua nchini alfajiri kuelekea mchezo wa raundi ya tatu dhidi ya Simba
Ni Jumapili Disemba 15 katika uwanja wa Benjamin Mkapa Simba na CS Sfaxien zitaumana mechi ya kusaka tiketi ya kutinga robo fainali
CS SFaxien wametokea Angola ambako juzi walichapwa mabao 3-2 dhidi ya Bravos. Watunisia hao wamepoteza mechi zote mbili za kwanza wakiburuza mkia kundi A
Ni wazi wameuchukulia mchezo huo dhidi ya Simba kwa umuhimu mkubwa pengine ndio sababu wamekuja nchini mapema
Hata hivyo watahitaji kufanya kazi ya ziada kuchukua alama mbele ya Simba ambayo pia imetoka kupoteza mchezo kule Algeria
Simba inazihitaji alama tatu za mchezo huo ili kuweka hai mkakati wao wa kufuzu robo fainali



