Kocha Mkuu wa Yanga Sead Ramovic amesema mchezo dhidi ya Mashujaa Fc utakuwa mgumu lakini jambo muhimu kwao ni kuhakikisha wanapambana kushinda ili kuweka hai malengo ya kutetea ubingwa ligi kuu kwa msimu wa nne mfululizo
Ramovic amesema hawawezi kutetea ubingwa kwa mazoea kwa kuwa wameshinda ubingwa mara nyingi. Kila mchezaji ana jukumu la kuhakikisha anajitoa kwa ajili ya kuisaidia timu kufikia malengo yake
"Itakuwa mechi ngumu lakini mimi kauli yangu ni moja tu, lazima twende tukapambane na kuonyesha tunastahili kuwa mabingwa kwa mara nyingine"
"Haitawezekana kuwa bingwa kama tutacheza kwa mazoea tukidhani itakuwa rahisi kwa sababu tumekuwa mabingwa mara nyinge," alisema Ramovic
Akizungumzia mkakati wake kuelekea mchezo huo, Ramovic amesema amefuatilia mechi zilizopita na aina ya mbinu ambazo wapinzani wao wamekuwa wakitumia hivyo amekiandaa kikosi chake kukabiliana na 'mitego' yao na kuhakikisha wanashinda
"Kwa nilichoona katika mechi zilizopita, timu nyingi zinapocheza dhidi yetu zinatumia mbinu ya kujilinda zaidi katika lango lao 'low block' na kushambulia kupitia mipira ya kushitukiza na wakati mwingine kujaribu kutuadhibu kupitia mipira ya kutenga"
"Tutacheza mechi hii kwa nidhamu kubwa tukihitaji kushinda, tutajaribu 'ku-press' tangu dakika ya kwanza na kuhakikisha hatuwapi wapinzani wetu nafasi ya kutudhuru"
Ramovic amesisitiza katika timu yake hakuna mchezaji star kila mmoja anapaswa kupambana katika uwanja wa mazoezi ili kupata nafasi ya kucheza
"Mimi nahitaji timu ya wachezaji 11, kila mchezaji lazima akimbie na aonyeshe anastahili kupata nafasi ya kucheza. Kama mchezaji alifunga mabao mengi au kutoa pasi nyingi za mabao misimu iliyopita, huu ni msimu mwingine tunapaswa kusahau yaliyopita, tunataka kuona kila mchezaji anafanya kazi yake vyema ili kuisaidia timu," aliongeza Ramovic



