Mnyama anarudi kileleni mwa msimamo wa ligi kibabe baada ya ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliopigwa uwanja wa Kaitaba, Kagera
Ilikuwa ni mechi ambayo Simba ilionyesha mapema kabisa kuzihitaji alama tatu na dakika 13 zilitosha kuandikisha bao la uongozi kupitia kwa Shomari Kapombe aliyemalizia krosi ya Mohamme Hussein 'Zimbwe Jr'
Simba iliendelea kutawala mchezo huo na dakika ya 44 ikaongeza bao la pili kupitia mpira wa adhabu uliopigwa Jean Charles Ahoua ambaye ameandikisha bao lake la sita msimu huu
Kipindi cha pili kocha wa Simba Fadlu Davids alibadili mfumo wa uchezaji wa kikosi chake wakiwaachia mpira Kagera Sugar watawale huku Simba ikitumia mashambulizi ya kushitukiza zaidi
Ulikuwa mtego ambao uliwanasa Kagera Sugar kwani kipindi cha pili Simba iliongeza mabao matatu huku Fabrice Ngoma akifunga bao lake la pili msimu huu na Steven Mukwala aliyeanzishwa mchezo wa leo badala ya Lionel Ateba akifunga mabao mawili akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Ladark Chasamb
Kagera Sugar ilifunga mabao yake dakika za lala salama kupitia kwa Datius Peter na Cleophas Mukandala
Simba inarudi kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha alama 34 huku ikiwa na mechi mbili za kiporo