Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imetupilia mbali rufaa ya Guinea dhidi ya Tanzania na hivyo kuipa uhakika Taifa Stars kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2025) nchini Morocco
Guinea ilikata rufaa hiyo baada ya mchezo namba 143 wa kuwania kufuzu Afcon baina yao na Tanzania uliochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Novemba 19, 2024 ikiitaka kamati ya nidhamu ya CAF kuiondoa Tanzania katika fainali za Afcon 2025 wakidai ilifanya kosa la kufoji kinyume na kanuni
Kwa mujibu wa rufaa hiyo, Guinea ilidai kuwa mchezaji Ibrahim Ame wa Tanzania aliyeingia kipindi cha pili kwenye mechi hiyo ambayo Tanzania iliibuka na ushindi wa bao 1-0 alikuwa na namba tofauti kwenye jezi kulinganisha na ile iliyopo kwenye fomu ya orodha ya wachezaji wa kutumika kwenye mechi hiyo
Guinea waliiomba kamati ya nidhamu ya CAF kuiengua Tanzania na kisha nafasi ya kucheza Afcon 2025 wapewe wao
Hata hivyo kamati ya nidhamu ya CAF iliyoketi Desemba 19, mwaka huu imeamua kuwa matokeo ya mchezo huo yabaki kama ilivyokuwa na Tanzania ibaki na haki ya kushiriki Afcon 2025
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Guinea (Feguifoot), imeeleza kuwa rufaa yao imetupiliwa mbali
"Kamati ya nidhamu ya CAF imekubali kwamba uhifadhi wa ushahidi uliofanywa na Shirikisho la Soka Guinea wakati wa mechi namba 143, Tanzania vs Guinea unakubalika katika fomu"
"Hata hivyo umekataliwa kwa vile hakuna hoja ya msingi," imefafanua taarifa hiyo ya Shirikisho la Soka Guinea
Mapema baada ya kusambaa kwa taarifa za Guinea kukata rufaa, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liliwatoa wasiwasi Watanzania kwa kufafanua kuwa taratibu zote zilifuatwa katika kumtumia Ibrahim Ame kwenye mchezo huo.