Licha ya kikosi chake kuhitaji sare tu dhidi ya Bravos ili kutinga robo fainali ya kombe la Shirikisho (CAF CC), Kocha Mkuu wa Simba Fadlu Davids amesema wanakwenda Angola kwenda kusaka alama tatu
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Simba iliandikisha ushindi wake wa kwanza ugenini msimu huu katika michuano ya kombe la Shirikisho (CAF CC) wakiichapa CS Sfaxien bao 1-0 katika mchezo uliopigwa Tunisia
Simba ilirejea jana kutoka Tunisia na wanatarajiwa kuondoka Dar mapema Alhamisi kuelekea Angola kwa ajili ya mchezo huo
Akizungumza muda mfupi baada ya kutua kutoka Tunisia, Fadlu alieleza furaha yake kwa vijana wake kupambana na kupata ushindi muhimu Tunisia
Fadlu alisema hesabu zao ni kushinda mchezo unaofuata ili kutinga robo fainali na kuhakikisha wanamaliza kwa ushindi mechi ya mwisho dhidi ya CS Constantine na kumaliza vinara wa kundi A
"Nina furaha baada ya kufanikiwa kupata ushindi ugenini Tunisia. CS Sfaxien ni moja kati ya timu kubwa barani Afrika, ina uzoefu, kwa hiyo haukuwa ushindi uliopatikana kirahisi"
"Uwanja pia haukuwa mzuri sana, lakini kikubwa tumepata matokeo ya ushindi. Kwa sasa tunahitaji sare ili tufuzu, ingawa hatutacheza ili kusaka sare, bali ushindi"
"Mechi ya mwisho tutataka tushinde ili tuongoze kundi, lakini haraka iwezekanavyo tunataka kufuzu kwenda robo, tutafanya kila linalowezekana lengo litimie," alisema Fadlu