Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025 inafikia tamati usiku wa leo wakati timu za taifa za Zanzibar Heroes, wenyeji wa michuano hiyo, na wageni Burkina Faso zitapovaana katika fainali ya kisasi kwenye Uwanja wa Gombani, visiwani Pemba
Zanzibar na Burkina Faso zinakutana tena kuanzia saa 1:00 usiku baada ya awali kuvaana katika mechi ya makundi na wageni kushinda kwa bao 1-0, hivyo leo ni zamu ya wenyeji kujitutuma na kulipa kisasi ili kuzuia taji la michuano hiyo lisiondoke nchini au iteleze tena na kuwa jamvi la wageni ikikosa kila kitu licha ya uenyeji wao.
Bingwa wa michuano hiyo iliyoanza tangu Januari 3 ikishirikisha timu za taifa badala ya klabu kama ilivyozoeleka atabeba ubingwa sambamba na zawadi ya Sh100 milioni, huku wageni wakionekana kuwa na nafasi nzuri kutokana na rekodi waliyoiweka hadi sasa ikiwa ndio timu pekee isiyoonja kipigo.