Baada ya kukamilisha malengo ya kuongoza kundi A katika michuano ya kombe la Shirikisho (CAF CC), kocha mkuu wa Simba Fadlu Davids alitoa mapumziko ya siku nne kwa wachezaji wake
Kesho kikosi cha Simba kinatarajiwa kurejea kambini kwa ajili ya mchezo wa Kombe la FA, pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tabora United unaotarajiwa kupigwa Februari 2, mwaka huu, katika Uwanja Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora
Jumapili Januari 26 Simba itamenyana na TRA Kilimanjaro katika mchezo wa raundi ya pili kombe la Shirikisho la CRDB kabla ya kusafiri mkoani Tabora kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tabora United
Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, amesema macho na hesabu zao wanazielekeza zaidi kwenye mchezo huo wa Februari 2 dhidi ya Tabora United
Ahmed amesema wanauchukuliwa kwa uzito mkubwa mchezo huo na watakwenda kwa tahadhari zote
"Tunakwenda kukabiliana na Tabora United, haitokuwa mechi nyepesi hata kidogo, lakini tutakwenda kwa ajili ya kupata matokeo mazuri"
"Sijajua ubora wa Tabora United uko wapi, ila ninachojua wanaweza kushinda michezo migumu, na kama ni hivyo hata sisi tunawajibika kwenda kwa tahadhari kubwa ili wasije kupata pia ushindi mbele yetu," alisema
Tabora United ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Yanga, Novemba 7, na kisha kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Singida Black Stars Novemba 25, kabla ya kuichapa Azam FC 2-1, Desemba 13, mwaka jana
Alisema kwa hali ambayo ligi imefika hawapaswi kudondosha hata pointi moja, hivyo hawako tayari kupoteza mchezo huo
"Katika ligi hii ilipofika ukiruhusu hata kupoteza pointi moja umesharuhusu mpinzani wako akufikie na kukupita kwa hiyo tunawajibika kuifunga Tabora na ni moja ya michezo migumu tuliyonayo mwezi Februari," alisema Ahmed