Dodoma Jiji yapata ajali Lindi

Joel JJ By Joel JJ β€’ 10th February 2025


Dodoma Jiji yapata ajali Lindi

Timu ya Dodoma Jiji imepata ajali ya basi ikitokea Ruangwa mkoani Lindi kuja jijini Dar es Salaam, baada ya jana tu kumaliza mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wao Namungo FC, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson amesema ajali hiyo imetokea katikati ya Nangurukuru na Somanga, huku akiweka wazi majeruhi ni wengi ila hakuna taarifa yoyote ya kifo hadi sasa.

"Basi lilipinduka mara mbili kwenye mto na wachezaji waliopata majeraha ya ajali ni wengi, tunashukuru tumepata msaada wa haraka sana wa kijiji na Serikali ya Mkoa wa Lindi ambao hadi muda huu tunapoongea wanaendelea kuwaokoa," amesema.

Fortunatus amesema kwa sasa ni mapema kuzungumza kile kinachoendelea ingawa baada ya muda watatoa taarifa kamili kwa kushirikiana na madaktari wa mkoa, hivyo mashabiki, wapenzi na wadau wa soka nchini waendelee kuwaombea majeruhi wote.

Dodoma Jiji ilikuwa safarini kuja Dar es Salaam kisha kwenda jijini Mbeya kwa ajili ya mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons uliopangwa kuchezwa Februari 14 kwenye Uwanja wa Sokoine


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.