Uongozi wa Tabora United, umefikia makubaliano ya kuachana na kocha mkuu wa timu hiyo, Anicet Kiazayidi huku nafasi yake ikichukuliwa na Mzimbabwe, Genesis Mangombe
Haijafahamika sababu za kuvunjwa kwa mkataba wa kocha huyo raia wa DR Congo ambaye hivi karibuni alirejea nchini kwao kwa ajili ya kufanya kozi ya refresh
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Tabora United, kimebainisha kuwa uongozi wa timu hiyo na kocha huyo wamefikia makubaliano ya pande zote mbili kuvunja mkataba
"Siwezi kuzungumza sababu za kuachana na kocha aliyepita ambaye ameisaidia timu yetu kuwa kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo hadi sasa, ninachoweza kusema ni makubaliano ya pande zote mbili"
"Hata tuliyemleta ni kocha mzuri, hivyo tunaamini atatuvusha katika malengo yetu kwa msimu huu kwani tunatamani kumaliza nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu," alisema mtoa taarifa huyo
Alipotafutwa Kocha Kiazayidi kuzungumzia suala hilo, alisema amefikia uamuzi huo kwa makubaliano ya pande mbili, huku akisita kueleza wazi kwa kina sababu zilizomfanya kuondoka ndani ya timu hiyo
Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Charles Obiny alisema kuna taratibu za kiuongozi zinaendelea juu ya hilo na zitakapokamilika wataweka wazi, hivyo mashabiki na wadau wa timu hiyo waendelee kuwapa sapoti kwa michezo ijayo
Tabora United ilimchukua Kiazayidi Novemba 2024 kuziba nafasi ya Mkenya Francis Kimanzi aliyeondolewa baada ya timu hiyo kuwa na mwenendo mbaya katika Ligi Kuu Bara msimu huu