Simba yatangaza kuifuata Al Masry Alhamisi

Joel JJ By Joel JJ β€’ 26th March 2025


Simba yatangaza kuifuata Al Masry Alhamisi

Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam Alfajiri ya Alhamis March 28 kuelekea Misri tayari kwa mchezo wa mkondo wa kwanza robo fainali ya kombe la Shirikisho (CAF CC) dhidi ya Al Masry utakaopigwa April 02 katika uwanja wa Suez

Akizungumza katika Mkutano na wanahabari mapema leo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ali amesema baadhi ya wachezaji ambao walikuwa katika timu ya Taifa ya Tanzania, wataunganisha moja kwa moja Misri

Ahmed amesema wanatambua mchezo dhidi ya Al Masry utakuwa mgumu lakini safari hii wamejipanga na lengo ni kuvuka hatua ya robo fainali

"Kikosi kitaondoka nchini alfajiri ya tarehe 28 kuelekea Misri kwa kutumia ndege ya Egypt Air. Wachezaji wetu waliokuwa Taifa Stars wataungana na timu nchini Misri. Camara na Mukwala tayari wamewasili nchini kujiunga na wachezaji wenzao kwa ajili ya maandalizi ya safari"

"Kila Mwanasimba atambue kwamba pamoja na mipango tuliyonayo lakini lazima tujipange, lazima tujiandae na hasa kama timu yenyewe inatokea Misri. Ukiangalia michuano ya Afrika ilivyo utaona kwamba Misri ndio nchi iliyoingiza timu nne kwenye robo fainali"

"Tunakwenda kucheza na Al Masry tukijua tunakwenda kucheza mechi ngumu kwelikweli lakini dhamira tuliyojiwekea ni kufuzu nusu fainali," alisema Ahmed

Ahmed amethibitisha Simba itamkosa beki wake Che Malone Fondoh ambaye anatibiwa majeraha ya goti nchini Morocco

Aidha Simba imetangaza viingilio vya mchezo wa marudiano ambao utapigwa April 09 katika uwanja wa Benjamin Mkapa ambao ulifanyiwa ukaguzi na maafisa wa CAF hivi karibuni

"Niwatoe hofu kwamba Uwanja wa Benjamin Mkapa umeshafanyiwa ukaguzi. Bado majibu hayajatoka lakini katika mazungumzo wanasema kuna maboresho makubwa kwenye uwanja ukilinganisha na mara ya mwisho walipofanya ukaguzi hivyo kuna nafasi kubwa ya kucheza kwenye uwanja huo"

"Na wote mnakumbuka kauli ya Msemaji Mkuu wa Serikali alivyosema kwamba uwanja upo tayari. Hatuna muda wa kusubiri tunafanya maandalizi"

"Viingilio vya mchezo dhidi ya Al Masry ni Mzunguko - 5,000, Orange - 10,000, Vip C - 15,000, Vip B - 30,000, Vip A - 40,000, Platinum - 150,000 na Tanzanite - 250,000. Tiketi zimeanza kuuzwa sasa"


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.