Jumatano April 02 katika uwanja wa Suez ulioko Mji wa Ismailia, wawakilishi pekee wa Tanzania waliobaki katika michuano ya CAF, Simba watatupa karata muhimu kuikabili Al Masry katika mchezo wa mkondo wa kwanza robo fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC)
Ni mechi ngumu lakini muhimu sana kwa Simba ugenini, kwani mechi hii inabeba hatma ya Mnyama kuvuka hatua ya robo fainali ambayo wamekwama kwa takribani misimu mitano mfululizo katika mashindano ya CAF
Al Masry ni moja ya timu ngumu katika michuano ya kombe la Shirikisho msimu huu licha ya kuwa walimaliza nafasi ya pili katika hatua ya makundi nyuma ya Zamalek iliyoongoza kundi D
Timu hiyo ambayo inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu ya Misri ilipoteza mechi moja tu hatua ya makundi
Rekodi za Al Masry katika ligi ya ndani zinaonyesha kuwa mchezo wa mwisho walitoka sare 1-1 na timu ya National Bank of Egypt
Kwenye mechi sita za makundi Masry, ilishinda mechi mbili nyumbani dhidi ya Black Bulls ya Msumbiji (3-1) na Enyimba ya Nigeria (2-0) kisha ikatoa sare tatu na kupoteza mmoja dhidi ya Zamalek (1-0)
Katika mechi tano zilizopita kwenye mashindano yote Al Masry wamelazimishwa sare tatu, kushinda moja na kupoteza moja
Hata hivyo wanakutana na Simba iliyo katika kiwango bora ikitoka kushinda mechi nne kati ya tano zilizopita
Simba inanolewa na kocha Fadlu Davids ambaye ana uzoefu wa kucheza mechi hizi za mtoano
Msimu wa 2021/22 Fadlu aliiongoza Orlando Pirates kucheza fainali ya kombe la Shirikisho ambapo katika mchezo wa robo fainali aliiondosha timu yake ya sasa Simba kwa mikwaju ya penati baada ya matokeo ya jumla ya sare ya bao 1-1
Msimu huu Simba imeweka malengo makubwa ya kucheza fainali ya michuano hiyo, ushindi au hata sare huko Misri itakuwa hatua moja muhimu kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa, April 09