Kikosi cha Simba leo kinaelekea Zanzibar kukamilisha maandalizi ya mchezo wa mkondo wa kwanza nusu fainali ya kombe la Shirikisho dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini utakaopigwa Jumapili, April 20 dimba la New Amaan Complex
Simba SC wataingia kwenye nusu fainali hii wakiwa na uzoefu mkubwa katika mashindano ya Afrika na rekodi nzuri wakiwa nyumbani
Miamba hao wa Msimbazi wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mashindano ya CAF, na kucheza Zanzibar ni kama nyumbani
Katika michuano hiyo msimu huu, ikiwa na kikosi chenye wachezaji wengi wenye damu changa wanaonolewa na kocha raia wa Afrika Kusini Fadlu Davids, Simba ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi ya kutwaa ubingwa
Stellenbosch FC, maarufu kama "Stellies", wanacheza nusu fainali yao ya kwanza kabisa kwenye Kombe la Shirikisho. Nao safari yao imekuwa ya kuvutia, wakivuka hatua mbalimbali kwa kuwatoa vigogo wa soka barani Afrika. Ulinzi wao madhubuti na mashambulizi ya kushtukiza yamekuwa silaha yao kubwa
Kwa kuzingatia uzoefu wa Simba SC na faida ya kucheza nyumbani, wanapewa nafasi kubwa ya kushinda mkondo wa kwanza
Hata hivyo ni wazi itakuwa mechi yenye ushindani, Stellenbosch FC ni timu isiyotabirika – ina nidhamu ya hali ya juu na wamedhihirisha wanaweza kufanya maajabu kama waliyofanya Misri kwa kuwatoa mabingwa watetezi Zamalek katika mchezo wa robo fainali
CAF tayari imemtangaza refa mzoefu Jean Jacques Ndala kutoka DR Congo ndiye amepangwa kuchezesha mechi hiyo ya kwanza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika
Ngambo mwenye umri wa miaka 37, amewahi kuichezesha Simba katika mechi nne tofauti za kimataifa ambapo imeshinda mbili, imetoka sare moja na kupoteza moja
Mechi ya kwanza kwa Ngambo kuichezesha Simba ilikuwa ni ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/2019 ambao ilipoteza kwa mabao 2-0 mbele ya JS Saoura ya Algeria ugenini
Refa huyo akachezesha mechi ya raundi ya kwanza ya ligi ya mabingwa Afrika msimu wa 2021/2022 ambayo Simba ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Msimu huohuo, Ndala alichezesha mechi ya nyumbani ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Mchezo wa mwisho kwa Ndala kuichezesha Simba ulikuwa ni ugenini wa mashindano ya African Football League ambao Simba ililazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly ya Misri.



