Kocha Mkuu wa Simba Fadlu Davids amewapongeza wachezaji wake kwa kufanikiwa kutinga fainali ya kombe la Shirikisho (CAF CC) baada ya matokeo ya suluhu ya bila kufungana dhidi ya Stellenbosch katika mchezo wa nusu fainali mkondo wa pili uliopigwa uwanja wa Moses Mabhida Jumapili jioni
Simba ilitinga fainali kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0 kufuatia matokeo ya ushindi hao katika mchezo wa mkondo wa kwanza
Akizungumza baada ya mchezo huo, Fadlu alisema wachezaji wamethibitisha wanaweza kubadilika na kuhimili kila aina ya mchezo
"Katika mechi zilizopita tulionyesha tunaweza kutawala mchezo na kuwalazimisha wapinzani wetu kukaa nyuma lakini leo tumeonyesha tunaweza kucheza hata bila ya mpira"
"Wachezaji wangu wameonyesha wanaweza kupambana hata katika mechi ambazo tutalazimika kukaa nyuma kuzuia"
"Nawaongeza kwa kile walichofanya leo (jana), tuko karibu kufikia malengo yetu"
"Kwa sasa tunaweza kufurahi lakini kwa kiasi kwa sababu bado hatujamaliza kazi. Tuna mechi mbili za fainali, furaha kubwa tutaipata mwisho," alisema Fadlu
Hii ni mara ya pili Fadlu anaiongoza timu kucheza fainali ya kombe la Shirikisho akifanya hivyo msimu wa 2021/22 akiiongoza Orlando Pirates
Lakini pia kwa mara nyingine anakwenda kukutana na RS Berkane katika mchezo wa fainali ambapo fainali iliyopita May 22 2022 Pirates walipoteza kwa mikwaju ya penati baada ya matokeo ya sare ya bao 1-1



