Kocha Mkuu wa Yanga Miloud Hamdi amesema wamepata muda wa kutosha kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Namungo Fc ambao utapigwa kesho Jumanne katika uwanja wa KMC Complex
Akizungumza katika mkutano na wanahabari mapema leo, Hamdi alisema umepita muda mrefu hawajacheza mechi ya ligi kuu hivyo malengo ni kuendeleza pale walipoishia
Hamdi amesema anafahamu Namungo Fc wanahitaji angalau alama moja kutoka mechi zilizobaki ili kujihakikishia kuendelea kucheza ligi kuu msimu ujao
Hivyo anajua wataingi katika mchezo huo wakiwa na lengo la kupata angalau droo lakini kwa Yanga huo ni mchezo ambao lazima washinde
"Nafurahi tumepata muda mrefu wa kujiandaa na mchezo huo. Mechi zilizopita tulicheza kila baada ya siku tatu lakini ukiangalia mara ya mwisho tulicheza mechi ya ligi kuu April 21"
"Hii ni mechi ambayo upande wetu ushindi ni matokeo ya lazima ili kuhakikisha tunaendelea kusalia kileleni katika msimamo wa ligi"
"Nafahamu Namungo Fc wanahitaji angalau alama moja tu ili kujihakikishia nafasi ya kubaki ligi kuu msimu ujao, hivyo sare yatakuwa matokeo mazuri kwao"
"Hatuna nafasi ya kufanya makosa katika mchezo huu, tunachohitaji ni ushindi, tofauti ya alama moja katika msimamo huku zikisalia mechi tatu inatulazimu kushinda kila mchezo ili kuweza kutimiza malengo yetu," alisema Hamdi
Akizungumzia hali ya kikosi, Hamdi amesema baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi kama Chadrack Boka, Khalid Aucho na Pacome Zouzoua wamerejea mazoezini na wenzao lakini hatma ya kutumika katika mchezo huo itategemea na utayari wao



