Mkufunzi wa Simba Fadlu Davids amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa mkondo wa kwanza fainali ya kombe la Shirikisho (CAF CC) dhidi ya RS Berkane ambao utapigwa Jumamosi, May 17 katika uwanja wa Manispaa ya Berkane
Akizungumza katika Mkutano wa mechi hiyo, Fadlu amesema licha ya kikosi chake kusheheni vijana wengi wadogo ambao hawana uzoefu mkubwa na michuano hiyo, wamejipanga kukabiliana na Berkane na lengo ni kupata matokeo mazuri katika mchezo huo
"Nawafahamu RS Berkane, tulicheza nao misimu michache nyuma wakati nikiwa na klabu ya Orlando Pirates. Ni timu yenye uzoefu mkubwa na michuano hii"
"Licha ya timu yangu kuwa na vijana wengi wadogo, tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri katika mchezo huu," alisema Fadlu
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini aliongeza kuwa wanafahamu wanakwenda kucheza mechi ya kwanza ya fainali hapo kesho na wiki ijayo kutakuwa na mechi ya pili ambayo Simba pia itakuwa na nafasi ya kutumia uwanja wa nyumbani
Kocha Fadlu ameeleza kuridhishwa na sehemu ya kuchezea (pitch) ya uwanja wa Manispaa ya Berkane na kuongeza kuwa watakuwa tayari kupeperusha vyema bendera ya Simba katika uwanja huo
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, beki Che Malone Fondoh amesema katika hatua waliyofikia hawaihofii timu yoyote na malengo yao ni kushinda mchezo huo
"Tumepata nafasi ya kucheza fainali, sisi kama wachezaji tunafahamu wajibu wetu, tunahitaji kushinda mchezo huu," alisema



