Kocha na mchezaji wa zamani wa klabu ya Simba SC, Jamhuri Kihwelo maarufu kama 'Julio', ametoa maneno ya matumaini na ushauri mzito kuelekea mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup) kati ya Simba SC na RS Berkane ya Morocco, utakaopigwa Jumapili hii, Mei 25.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Morocco, Simba walijikuta wakifungwa mabao 2-0 — matokeo ambayo yamewapa kazi ya ziada katika mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, Julio haoni kama yote yamekwisha. Kwa macho ya uzoefu na uelewa wa soka la Afrika, anaamini Simba bado wana nafasi.
"Hata kama tusingefungwa, huu ni mchezo mgumu. Bado kazi ni kubwa kwa sababu na wao wanataka ubingwa kama sisi," Julio alisema.
Kocha huyo amesisitiza kuwa Berkane walitumia makosa ya Simba kwa ustadi mkubwa na kupata mabao yao. Lakini sasa, anaamini benchi la ufundi la Simba limeona na kuchambua makosa hayo, na tayari wameyafanyia kazi kuelekea mechi ya Jumapili.
"Wametumia makosa yetu na kupata mabao mawili, lakini sasa nasi tunahitaji kurekebisha hayo makosa ili tupate ushindi hapa nyumbani, kama ilivyokuwa dhidi ya Al Masry," aliongeza Julio.
Kocha Julio anaamini kuwa pambano la Jumapili litakuwa mtihani wa tabia, maarifa, na moyo wa Simba SC. Hili si tu suala la mbinu, bali pia ni vita ya kiakili na hisia. Simba wana kazi kubwa mbele yao — lakini historia ya timu hiyo imejaa ushindi mkubwa katika mazingira magumu.
“Naamini makosa yaliyofanyika yameonekana na kufanyiwa kazi. Kwa hiyo, kuna jambo litafanyika na tutapata matokeo mazuri na kutwaa ubingwa wa mashindano haya,” Julio alihitimisha.