Wakati msimu wa ligi kuu ukitarajiwa kufika tamati mwezi ujao, tayari michakato ya usajili inaendelea kwa nyota ambayo mikataba yao inaelekea ukingoni
Taarifa kutoka Yanga ni kuwa klabu hiyo ilianza mapema michakato ya kuhuisha mikataba ya wachezaji wake ambayo inamalizika mwishoni mwa msimu
Mpaka sasa wachezaji kama Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Dickson Job tayari wameramba mikataba mipya huku wachezaji wengine kama Khalid Aucho na Clatous Chama mazungumzo yakiwa yanaendelea
Hata hivyo kwa upande wa Chama imeelezwa kiungo huyo wa zamani wa Simba amepewa ya mkataba wa mwaka mmoja ambao thamani yake imezingatia mchango wake katika kikosi cha Yanga msimu huu
Kuna taarifa pia waajiri wake wa zamani Simba wanapambana kutaka kumrejesha kiungo huyo aliyejijengea heshima kubwa katika soka la Tanzania
Katika msimu wake wa kwanza na Yanga, Chama amekuwa na wakati mgumu kupenya katika kikosi cha kwanza mbele ya Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua ambao wamekuwa katika ubora mkubwa
Chama amefunga mabao manne na kutoa asisti mbili katika ligi kuu ya NBC ambazo zaidi ya asilimia 80 ya mechi alizocheza, alitokea bench
Hata hivyo baada ya Aziz Ki kuondoka, pengine ni nafasi yake kurejea katika kikosi cha kwanza lakini pia msimu ujao eneo analocheza linatarajiwa kuwa na ushindani zaidi kwani Yanga inatarajiwa kusajili kiungo mwingine kuchukua nafasi ya Aziz Ki