Klabu ya Yanga imeweka bayana yale yaliyozungumzwa baina yake na Bodi ya ligi katika kikao kilichofanyika mapema leo
Akizungumza na wanahabari Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema Mtendaji wa Bodi Almas Kasongo amepotosha baadhi ya masuala yaliyojadiriwa katika kikao hicho
Kamwe amesema ni kweli Yanga imetaka mambo manne yafanyiwe kazi kabla ya kukubali kucheza mechi namba 184 dhidi ya Simba
Katika mambo hayo manne, matatu ni lazima yafanyiwe kazi sasa na moja litahitaji muda hadi kukamilishwa
“Ni kweli tulipokea barua ya wito Juni 7 na leo tumeshiriki kikao kama tulivyoombwa na bodi ya Ligi kwenye kikao hiki maalum ambacho hakikuwa cha maandalizi ya mechi bali ni kujadili sintofahamu ya mchezo namba 184 wa Ligi Kuu”
“Kwenye kikao chetu tuliuliza pia kuhusu ripoti ya kilichotokea Machi 8, na CEO wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo akakiri kuwa ripoti wanayo na kuna kiongozi mkubwa wa Serikali alipiga simu kuzuia geti la uwanja lisifunguliwe, lakini hawawezi kumtaja hadharani. Nashangaa hili hajalisema kwenye tuliyoyazungumza leo, tumshauri akiamua kusema aseme yote asibakishe”
“Tumetoa matakwa manne. Matatu yanahusu mchezo namba 184, tunaamini yakifanyiwa kazi hayo matatu kwanza, tutakuwa tayari kucheza mechi hiyo kwa tarehe nyingine itakayopangwa. Na takwa la nne ni la muda mrefu, kuanzia msimu ujao. CEO wa Bodi ya Ligi Almasi Kasongo asiudanganye UMMA kwa kuchagua kuzungumzia takwa moja tu na kuacha yanayotakiwa kushughulikiwa kwa haraka ikiwemo yeye mwenyewe kujiuzulu”
“Takwa letu la kwanza na la pili linahusu ukiukwaji wa kanuni uliofanyika Machi 8. Tunataka Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi pamoja na CEO wa Bodi ya Ligi Almasi Kasongo wawajibike kwa kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia kanuni na kuutia doa mpira wetu. Ligi yetu ni kubwa sana Afrika na inataka watu makini wenye weledi kuiongoza”
"Takwa letu la tatu ni kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya maamuzi mabovu ya mara kwa mara ya waamuzi. Kamati ya waamuzi ipo chini ya TFF kwa Katibu Mkuu, unashangaa ni vipi mwamuzi mmoja anafanya makosa yakujirudia na bado anaendelea kupangwa kwenye mechi bila kuchukuliwa adhabu yoyote ile"
"Napenda kuwajuza waandishi wa Habari, yasipofanyiwa kazi matakwa yetu matatu kwa uharaka, Young Africans SC hatutakuwa tayari kucheza mchezo namba 184, mechi zote mbili za Ligi zilizobaki na hatutashiri Ligi Kuu Msimu ujao. Huu ndio msimamo wetu na hatutayumba kwa lolote lile,” alisema Kamwe