Uongozi wa Simba umeendelea 'kupiga kimya' kuhusu mchezo wa ligi kuu dhidi ya Yanga ambao umepangwa kupigwa Juni 25 2025
Zikiwa zimesalia siku mbili kuelekea mchezo huo, hakuna kiongozi yeyote wa Simba ambaye amekuwa tayari kuzungumzia mchezo huo licha ya Kocha Mkuu Fadlu Davids kuthibitisha kukiandaa kikosi chake kwa ajli ya mchezo huo utakaopigwa Jumatano
Akizungumza baada ya mchezo wa mwisho nyumbani dhidi ya Kagera Sugar ambao Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0, Fadlu alidokeza mabadiliko ya kikosi aliyofanya yalizingatia mkakati wa mechi hiyo ya dabi ya Kariakoo
Hata hivyo Mwenyekiti wa Simba Murtaza Mangungu hakuwa tayari kuzungumzia mchezo huo akisisitiza Simba ni klabu ya mpira wa miguu hivyo kazi yao ni kucheza mpira na hawaihofii timu yoyote
Alipoulizwa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ali alisema jana Simba ilicheza mechi yake ya mwisho katika uwanja wa nyumbani, kama kutakuwa na lolote kuhusiana na mechi hiyo Wanasimba watataarifiwa
"Ratiba inapotoka huhitaji kuthibitisha kama unacheza au la bali unaanza maandalizi kueleke mechi husika. Na mimi nichukue nafasi hii kuwaambia wanasimba taarifa rasmi ni kwamba kama kutakuwa na lolote kuhusiana na mechi ya tarehe 25, tutawaeleza"
"Lakini kwa sasa niseme kwamba tumecheza mchezo wetu wa mwisho nyumbani wa ligi kuu ya NBC 2024/25," alisema Ahmed