Klabu ya Fountain Gate FC imefanikiwa kusalia kwenye Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 5-1 dhidi ya Stand United katika michezo miwili ya mtoano (play-off).
Katika mchezo wa marudiano uliochezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara, Fountain Gate ilionyesha dhamira ya kusalia ligi kuu kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Ushindi huo ulihitimisha jumla ya mabao 5-1, baada ya kuibuka na ushindi wa 3-1 kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa mjini Shinyanga.
Kwa matokeo haya, Fountain Gate wanabaki katika Ligi Kuu kwa msimu ujao wa 2025/26, wakijihakikishia nafasi yao miongoni mwa vigogo wa soka la Tanzania Bara.
Kwa upande wa Stand United, ndoto yao ya kurejea ligi kuu imeyeyuka baada ya kushindwa kuonyesha makali katika michezo yote miwili ya mtoano.
Klabu hiyo itasalia kwenye Ligi ya Championship kwa msimu mwingine, huku ikilazimika kujipanga upya kwa kampeni za kupanda daraja msimu ujao.
Fountain Gate watatumia muda huu kujiimarisha zaidi kwa ajili ya msimu mpya, wakijifunza kutoka kwenye changamoto za msimu uliomalizika ili kuepuka hali kama hiyo katika kampeni zijazo.



