Mshambuliaji wa Yanga SC, Clement Mzize, bado yuko njia panda kuhusu hatma yake ya kutua klabu ya Zamalek ya Misri, licha ya awali kuonekana kama dili lililokamilika.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vya karibu na mchezaji huyo, tayari Yanga ilikuwa imekubaliana na Zamalek kuhusu uhamisho wake, lakini mvutano wa kimaslahi kati ya wasimamizi wa Mzize na klabu hiyo ya Cairo umechelewesha dili hilo.
Mzize, ambaye msimu uliopita aliibuka kuwa mmoja wa wafungaji bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufunga mabao 14, yakiwa mawili nyuma ya kinara Jean Charles Ahoua wa Simba SC, ameendelea kuvutia vilabu vya nje, ikiwemo Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Hata hivyo, tetesi za uhamisho wake Kaizer Chiefs zinaonekana kufifia, hasa baada ya klabu hiyo kuanza rasmi maandalizi ya msimu mpya (pre-season) bila uwepo wa mshambuliaji huyo.
Iwapo sintofahamu kati ya wasimamizi wa Mzize na Zamalek haitatatuliwa hivi karibuni, kuna kila dalili kuwa mshambuliaji huyo atasalia Jangwani kwa msimu mwingine akiwa bado na mkataba wa miaka miwili na Yanga
Mzize yuko na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kilichoweka kambi Misri kujiandaa na michuano ya CHAN inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani inayoanza August 02 na kufikia tamati August 30