Yanga inatarajiwa kutumia michuano ya CHAN 2024 itakayoanza August 02 hadi August 30 kusaka wachezaji mahiri wa kuwasajili, imefahamika
Akizungumza hivi karibuni, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe alisema usajili wa timu hiyo umekamilika kwa asilimia 85
Kigogo mmoja wa Yanga amenukuliwa na Mwanaspoti, akibainisha kuwa wataacha nafasi chache ili kuangalia wachezaji wengine kwenye michuano ya CHAN akieleza shida kubwa ni kupata mastaa wenye ubora lakini suala la fedha si tatizo kwao.
Kwa mujibu wa bosi huyo, walichopanga ni kwa baadhi ya nafasi wanazotaka kuziboresha kwenye kikosi chao watakuwa na mkakati maalum wa kuangalia watu bora watakaopatikana kwenye fainali hizo.
Bosi huyo wa juu Yanga anayehusika kwenye usajili, alisema wachezaji wote wanaoshiriki fainali hizo, ni wale wanaocheza ligi za ndani Afrika, hivyo wanaona hakutakuwa na ugumu mkubwa kwao kuwapata.
“Hatuwezi kumaliza nafasi zote, tutakuwa na jicho letu kwenye hizi Fainali za CHAN, unajua shida yetu sisi ni watu bora tunaowataka, sio fedha"
“Kama ingekuwa fedha tusingeingia sehemu ambazo kuna timu unaambiwa inazunguka na mchezaji ikiongea naye, tunataka watu sahihi kwa malengo yetu"
“Kuna wachezaji tutawatafuta kwenye fainali hizi, tumejipanga kwenda Uganda, Kenya na hapa nchini kufuatilia kwa kina wachezaji bora tunaowataka,” alisema
Michuano hiyo inafanyika katika kipindi ambacho dirisha la usajili liko wazi kwani litafungwa Septemba 7 huku michuano hiyo ikitarajiwa kufika tamati August 30



