Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' imeanza vyema mashindano maalumu ya CECAFA ya kujiandaa na Michuano ya CHAN 2024 baada ya kuichapa Uganda kwa bao 1-0
Huu ulikuwa mchezo maalumu wa maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) ambao umepigwa kwenye Uwanja wa Black Rhino Karatu Mkoani Arusha.
Awali mashindano hayo yalikuwa yanashirikisha timu za Tanzania, Kenya, Uganda na DR Congo, lakini Kenya na Congo zilijitoa huku Senegal ikipewa nafasi ya kushiriki.
Katika mchezo huo, ambao ulihudhuriwa na mashabiki wengi, Stars ilionekana kucheza soka zuri kipindi cha kwanza na kufanikiwa kujipatia bao la mapema lililowekwa kimiani na Iddi Nado katika dakika ya 13 tu ya mchezo huo.
Kabla ya bao hilo, wachezaji wa Stars walipigiana pasi kutoka langoni kwao na mpira ulimfikia mfungaji ambaye alipiga shuti kali kutoka nje ya eneo la 18 na kumshinda kipa wa Uganda.



