Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco', amesema kikosi chake kimekamilika kwa asilimia 80, na kwamba zilizobaki atazimalizia siku chache kabla ya kuanza fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), Jumamosi wiki hii.
Akizungumza juzi baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Timu ya Taifa ya Senegal, ukiwa ni maalum kujiweka sawa kabla ya fainali za CHAN, zinazofanyika hapa nchini kwa ushirikiano na nchi za Kenya na Uganda, Morocco, alisema pamoja na ushindi walioupata, lakini bado timu yake ina mapungufu machache, ambapo atatumia siku chache zilizobaki kuyarekebisha.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Black Rhino, Karatu mkoani Arusha, Stars ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Senegal, yakiwekwa wavuni na Abdul Suleiman Sopu na Ibrahim Hamad 'Bacca'.
"Tumemaliza mechi salama na tumefanikiwa kwa asilimia 80 kwa kile ambacho tulikipanga katika mechi hizi mbili tulizocheza huku."
"Bado kuna mambo hayajakaa vizuri, kuna maeneo ambayo tunahitaji kuyafanyia kazi, kabla hatujaanza mechi yetu ya ufunguzi wa CHAN Agosti 2," alisema Morocco.
Aliwahakikishia Watanzania kuwa hadi kufikia Jumamosi kila kitu kitakuwa tayari na wanatarajia kufanya vizuri katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Burkina Faso, utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
"Tunaendelea kujipanga, tunarudi nyumbani, tuna siku nne za kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza kwenye michezo hii miwili, japo tumeshinda, nadhani mpaka siku hiyo tutakuwa vizuri," alisema.
Ulikuwa ni mchezo wa pili kwa Stars kushinda, ambapo Jumanne iliyopita, ikiwa kwenye uwanja huo, ilitoa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Uganda Cranes, lililowekwa ndani ya wavu na Idd Selemani 'Nado', katika michuano maalum ya kujiandaa na fainali, iliyopewa jina la CECAFA 3 Nations Pre-CHAN.
Kikosi cha Stars kimerejea Dar es Salaam, kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo wa ufunguzi, Jumamosi ijayo.



