Stars jino kwa jino na Burkina Faso ufunguzi CHAN 2024

Joel JJ By Joel JJ • 2nd August 2025


Stars jino kwa jino na Burkina Faso ufunguzi CHAN 2024

Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) yanatarajiwa kuanza rasmi leo , Agosti 02, 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ambapo Tanzania (Taifa Stars) itamenyana na Burkina Faso katika mchezo wa ufunguzi utakaoanza saa 2:00 usiku.

Tanzania inakuwa mwenyeji wa mashindano haya kwa mara ya kwanza katika historia, kwa kushirikiana na Kenya na Uganda kama waandaaji wenza wa michuano hiyo ya Afrika.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa na ushindani mkali, huku makocha wa timu zote mbili wakiweka wazi dhamira zao kuelekea mchezo huo

Mkufunzi wa Stars Hemed Morocco amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono akiwahakikishia kikosi chake kiko tayari kwa michuano hiyo

"Tupo Tayari, Tuna Kikosi imara. Tupo tayari kukutana na timu yoyote katika mashindano haya kutokana na aina ya kikosi nilichonacho. Tumefanya maandalizi ya kutosha na wachezaji wote wako fiti,” alisema Morocco katika mkutano na wanahabari

Kocha huyo ameongeza kuwa michezo ya kirafiki waliyocheza kabla ya mashindano imesaidia kupunguza presha kwa wachezaji, hasa chipukizi waliopo kwenye kikosi hicho.

“Wachezaji chipukizi wameonyesha kiwango kizuri na kushirikiana vyema na wazoefu. Tunaamini tunaweza kufanya vizuri na kuacha kombe nyumbani,” alisisitiza.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, mlinda lango Aishi Manula alisema wanakwenda kupambana kulinda heshima ya nchi nyumbani

"Tutapambana Kulinda Heshima ya Nyumbani.Tunajivunia kucheza kwenye ardhi ya nyumbani. Tutapambana kuhakikisha tunashinda michezo yetu ya mwanzo,” alisema Manula. 


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.