Yanga, Wakala wavutana ofa za Mzize

Joel JJ By Joel JJ β€’ 11th August 2025


Yanga, Wakala wavutana ofa za Mzize

Sakata la usajili wa mshambuliaji wa Yanga SC, Clement Mzize, limechukua sura mpya baada ya viongozi wa klabu hiyo kuweka wazi msimamo wao: hawatauza mchezaji kwa mapendekezo ya wakala wake, bali kwa kuzingatia thamani halisi ya mchezaji katika soko na muda uliopo.

Jana, klabu ya Esperance kutoka Tunisia iliwasilisha ofa rasmi Jangwani kwa ajili ya kumsajili Mzize, lakini mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara waliikataa mara moja.

Ikumbukwe kuwa Yanga tayari walikuwa wamekubaliana na klabu ya Umm Salal ya Qatar kumuuza Mzize kwa kiasi cha dola 900,000. Hata hivyo, dili hilo limesimama kutokana na kutokuwepo kwa makubaliano binafsi kati ya mchezaji na klabu husika, chanzo kikuu kikiwa ni msimamo wa wakala wa Mzize ambaye hataki mteja wake ajiunge na timu hiyo ya Qatar.

Badala yake, wakala huyo alipendekeza Yanga wamruhusu Mzize kujiunga na Al Masry ya Misri, ingawa klabu hiyo iliwasilisha ofa ndogo ya dola 600,000, chini kwa kiasi kikubwa ya thamani iliyowekwa na Yanga.

Vyanzo vinaeleza kuwa wakala huyo hana uhusiano mzuri na uongozi wa Yanga, hali iliyochochea mivutano ya mara kwa mara. Hata pale Zamalek SC walipoonyesha nia ya kumsajili Mzize, mpango huo ulisitishwa baada ya gharama upande wa mchezaji kuongezeka kinyume na makubaliano ya awali.

Kwa sasa, hatma ya Mzize inasalia kuwa yenye sintofahamu, huku Yanga wakisisitiza kuwa maslahi ya klabu na heshima ya mchezaji ndiyo kipaumbele na si masharti ya wakala.


  

XTRA 90 INSIDER

Get the latest tactics & rumors delivered to your inbox.