Kocha Mkuu wa Simba Fadlu Davids amesema kikosi chake kimeanza kuonyesha mabadiliko ya kiuchezaji baada ya wiki mbili za pre-season katika mji wa Ismailia, Misri
Jana Simba ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu inayoshiriki ligi kuu ya Misri, Kahraba Ismailia, mchezo uliomalizika kwa Mnyama kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyowekwa kambani na Mohamed Bajaber na Jonathan Sowah katika kila kipindi
Akizungumza baada ya mchezo huo, Fadlu alibainisha kuwa kikosi chake kimeonyesha mambo mengi mazuri baada ya muda mfupi wa mazoezi waliyofanya hapo Misri
"Tumecheza dhidi ya timu nzuri, mechi ilikuwa na ushindani, ukifanya tathmini tangu mechi yetu ya mwisho msimu uliopita na tulipo sasa, utaona tumepiga hatua"
"Ukiangalia kipindi cha kwanza ukitoa golikipa na wachezaji wengine wachache, tulianza na wachezaji wengi wapya lakini waliweza kucheza kwa kuzingatia mfumo wetu"
"Kipindi cha pili tulibadili timu nzima, ni mchezaji mmoja tu ambaye aliendelea kutoka kipindi cha kwanza, tuliendelea kucheza vizuri wachezaji waliongeza kasi na morali ya timu kwa ujumla"
"Ni mechi ambayo tungeweza kufunga mabao zaidi pengine matatu au manne, nimeridhika lakini bado hatujamaliza, tuna kazi ya kufanya kwenye uwanja wa mazoezi," alisema Fadlu
Kikosi cha Simba kitaendelea kujifua Ismailia kwa siku chache zaidi kabla ya kuelekea Cairo ambapo watacheza mechi zaidi ya kirafiki



