Kocha Mkuu wa Simba Fadlu Davids ameridhishwa na kiwango cha kiungo Naby Camara raia wa Guinea na hivyo fundi huyo wa mpira anatarajiwa kupewa mkataba wa miaka miwili kuwatumikia Wekundu hao wa Msimbazi, imefahamika
Camara aliwasili Ismailia wiki iliyopita Fadlu akihitaji kumfuatilia mazoezini kabla ya kuidhinisha usajili wake
Nyota huyo aliyewahi kuitumikia CS Sfaxien, juzi alipata nafasi ya kucheza mchezo wake wa kwanza wa kirafiki wa kujipima nguvu dhidi ya Kahraba Ismailia, ikishinda kwa mabao 2-0 mabao yakifungwa na kiungo Mohammed Bajaber na mshambuliaji Jonathan Sowah.
Camara kwenye mchezo huo alipewa dakika 45 akionyesha kiwango kizuri, akicheza kama kiungo mkabaji kabla ya kubadilishwa na kupumzishwa. Camara pia anamudu kucheza nafasi ya beki wa kushoto na hata mlinzi wa kati
Fadlu amehitaji kuongeza nguvu eneo la kiungo mkabaji na beki wa kushoto, kumpata Camara ambaye anamudu kucheza nafasi zote mbili ni faida kwake
Aidha beki wa kushoto Hernest Malonga nae yuko Ismailia akisubiri hatma yake baada ya kujifua na kikosi cha Simba kwa takribani wiki moja