Wakati Simba ikichuana na Gor Mahia jana katika mchezo wa kirafiki maalum kuhitimisha Tamasha la Simba Day, mashabiki wa Simba walikuwa makini kuangalia viwango vya nyota wapya waliosajiliwa katika dirisha hili
Kwa ujumla Wanasimba walionekana kuridhishwa na viwango vilivyoonyeshwa na wachezaji wote wapya waliopewa nafasi katika mchezo huo ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 hasa ikizingatiwa ulikuwa mchezo wa kwanza kuwashuhudia nyota hao
Lakini wapo wachezaji miongoni mwao ambao waliacha tabasamu kwa mashabiki kwa kile walichoonyesha katika mchezo huo
Beki kisiki Rushine De Reuck aliyetua Simba kutoka klabu ya Mamelodi Sundowns ni miongoni mwa wachezaji hao
Kama ni kupewa alama kulingana na kazi aliyofanya uwanjani, basi De Reuck angeweza kuondoka na alama 9 kati ya 10
Mahiri katika kupiga pasi, katika pasi 80 alizopiga, 78 zilifika kwa usahihi. De Reuck alicheza mipira ya hatari 10 huku akifanikiwa kupiga mipira mirefu 4 iliyofika
De Reuck alionyesha umahiri wake katika kuzima mashambulizi na kuanzisha mipira kwa pasi zake zilizonyooka mithiri ya rula
Ni wazi ujio wake unakwenda kuimarisha eneo la safu ya ulinzi na pengine huenda akawa beki tegemeo katika eneo hilo akishirikiana na Abdulrazak Hamza na Carabou Chamou huku pia Wilson Nangu na Masinde wakitarajiwa kuwapa changamoto mabeki hao