Kiungo mahiri wa Azam FC na Timu ya Taifa ya Tanzania, Feisal Salum Abdallah "Fei Toto", ameongeza mkataba mpya wa mwaka mmoja kuendelea kuichezea timu hiyo hadi mwaka 2027.
Feisal, ambaye alitikisa dirisha la usajili baada ya kuhusishwa kwa muda mrefu na klabu ya Simba SC, sasa amefuta uvumi huo kwa kusalia Chamazi. Hatua yake imezima matumaini ya mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi waliokuwa wakitamani kumuona akivaa jezi nyekundu msimu ujao.
Kwa muda mrefu, tetesi zilielekeza kwamba kiungo huyo alikuwa chaguo namba moja kwa Simba SC, hasa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza katikati ya uwanja, kutuliza mchezo, na kusambaza pasi sahihi. Hata hivyo, uongozi wa Azam FC umeonyesha dhamira ya dhati ya kuendelea kumtumia kama mhimili wa timu yao.
Kwa kuongeza mwaka mmoja zaidi, Feisal sasa anabaki kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Azam FC kinachojiandaa kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na michuano ya kimataifa.