Rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said, ameendelea kuthibitisha hadhi yake kama kiongozi wa mafanikio makubwa baada ya jana kushuhudia timu yake ikinyakua taji la kwanza la msimu huu.
Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya watani wao wa jadi Simba SC katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Hilo lilikuwa taji la sita kwa Yanga ndani ya kipindi cha misimu miwili, na la nne la Ngao ya Jamii katika misimu mitano. Kwa hesabu ya jumla, Yanga imekusanya zaidi ya mataji 16 ndani ya miaka minne tangu Hersi alipotua na kuchaguliwa kuwa Rais wa klabu, jambo linalodhihirisha upeo wake wa kiuongozi na ufanisi katika kutengeneza kikosi imara.
Zaidi ya mafanikio ya makombe, ushindi dhidi ya Simba jana uliendeleza rekodi adimu kwa Yanga, kwani huo ulikuwa ni ushindi wa sita mfululizo dhidi ya watani wao hao wa jadi.
Hii ni rekodi inayozidi kuimarisha nafasi ya Hersi kama kiongozi anayejua kusimamia mikakati, kuanzia usajili wa wachezaji hadi maandalizi ya ushindi uwanjani.
Kwa hali ilivyo sasa, ni sahihi kabisa kusema: Hersi Said ni Rais wa Makombe wa Yanga, kiongozi ambaye ameweka alama kubwa na kuandika ukurasa mpya wa historia ndani ya klabu hiyo kongwe ya Tanzania.






