Kocha Mkuu wa Yanga Romain Folz amesema amekiandaa kikosi chake kwenda kupambana huko Malawi ili kuhakikisha wanaanza vyema mechi ya mkondo wa kwanza kuwania kutnga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa (CAFCL) dhidi ya Silver Strikers
Yanga inatarajiwa kuondoka nchini kesho Alhamisi kuelekea Malawi ambapo mchezo huo utapigwa siku ya Jumamosi, Oktoba 18
Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake, Folz amesema hakuna mechi nyepesi katika michuano ya ligi ya mabingwa hivyo wamejipanga kukabiliana na timu ngumu kama ilivyokuwa mchezo uliopita dhidi ya Wiliete Sc
"Tumekuwa na maandalizi mazuri pamoja na kuwa katika kipindi hiki cha mapumziko ya FIFA tumewakosa baadhi ya wachezaji lakini niseme tumepata wakati mzuri wa kujiandaa na tuko tayari kukabiliana na mpinzani anayekuja mbele yetu"
"Hii ni ligi ya mabingwa hivyo hatutarajii mechi nyepesi kama ilivyokuwa mechi iliyopita dhidi ya Wiliete Sc. Tumepata muda wa kuwafuatilia Silver Strikers, ni timu nzuri tunajua ni mkakati gani tunapaswa kwenda nao Malawi"
"Muhimu kabla ya kufikiria nini tunakwenda kufanya, jambo la kwanza ni kumuheshimu mpinzani na kuwa tayari kukabiliana nae huku tukiweka malengo ya kushinda," alisema Folz
Folz amesisitiza kuwa timu yake itaendelea kuwa na mabadiliko na kuimarika siku hadi siku jambo muhimu akiwataka mashabiki kuwa na imani juu ya kazi inayofanywa na benchi la ufundi
"Kama nilivyosema mwanzo, hii sio kazi ya siku moja, nafurahi kuona tunaendelea kuimarika na naamini tutaendelea kuwa bora siku hadi siku"