Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema wachezaji wake wana morali kubwa kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Al Ahly ambao utapigwa Ijumaa, Januari 23 huko Misri.
Akizungumza na wanahabari mapema leo muda mfupi kabla ya kuondoka nchini, Goncalves alisema licha ya kukabiliwa na safari ndefu lakini wanakwenda Misri wakiwa na ari kubwa.
"Hatutakuwa na muda mrefu wa maandalizi lakini nikwambie wachezaji wangu wana ari kubwa kuelekea mchezo huo"
"Tutasafiri kwa ndege hadi Cairo kisha tutapanda basi hadi mji wa Alexandria, muda ni mfupi lakini tumeshajiandaa hapa"
"Sasa tuna timu iliyoimarika zaidi ambayo inatupa nafasi ya kushindana na timu bora kama Al Ahly. Wachezaji wote tulisafiri nao wako tayari na tunakwenda kuipambania nembo ya Yanga," alisema Goncalves.
Yanga itasafiri kwa takribani masaa tisa ambapo masaa matano watakuwa angani hadi Cairo ambapo hapo watachukua usafiri wa basi kuelekea mji wa Alexandria takribani masaa manne.
Mchezo dhidi ya Al Ahly utapigwa Ijumaa, saa 1 usiku kwa saa za Tanzania.
Yanga iliondoka mapema leo ikiwa na kikosi kilichojumuisha wachezaji 24.



