Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema heshima waliyonayo kwa klabu ya Al Ahly ni kutokana na mafanikio yao makubwa katika soka la Afrika lakini hawahofii kukabiliana nao kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa hapo kesho.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, Goncalves amesema ili wafikie kiwango cha juu lazima wacheze na kupata ushindi dhidi ya timu bora.
Amesema Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na dhamira ya kupata ushindi. Ubora wa kikosi chake na ari ya timu inampa matumaini ya kufanya vyema katika mchezo huo.
"Tunatambua kuwa tunacheza dhidi ya klabu kubwa zaidi Afrika, klabu ya karne na hilo linahitaji heshima. Lakini kama tunataka kuwa sehemu ya historia ya soka la Afrika, si suala la kuwa na hofu ni suala la kucheza mpira. Mwisho wa siku tunakuja kucheza na kujaribu kuwashinda wapinzani wetu, huo ndio mpango wetu wa kesho."
"Ili ufikie kiwango cha juu lazima ucheze dhidi ya timu bora. Tunaamini kikosi chetu kina ubora, wachezaji wana kiwango na wana hamu ya kutoa kila kitu kwa ajili ya timu. Tunawaamini wachezaji wetu na tunaamini kuwa kesho tutapata matokeo tunayoyataka"
"Kundi letu ni gumu sana. Tunawaheshimu wapinzani wetu wote kwa sababu wana historia kubwa na wametwaa mataji mengi barani Afrika. Lakini ukweli ni kwamba sisi pia tunakua na tuna mipango ya muda mrefu ya kuwa miongoni mwa timu bora Afrika."
"Baada ya mechi mbili tayari tuna pointi nne na bado tuna nafasi nzuri ya kuvuka hatua ya makundi. Lengo letu sasa ni kufuzu kutoka kwenye kundi. Haitakuwa rahisi lakini tumejiandaa vizuri na tunaamini tunaweza kufanikiwa"
"Kila mechi tunaingia kwa lengo la kushinda. Huo ndio mtazamo wetu. Tuko kwenye mchakato wa maendeleo, na tangu nilipojiunga na timu, tumepiga hatua kubwa. Matokeo yanaonyesha hilo, lakini muhimu zaidi ni maendeleo ya jumla ya timu."
"Kuhusu wachezaji, tunataka kila mmoja ajisikie kama yuko nyumbani. Tuna malengo ya pamoja na ndoto za kufanikisha mambo makubwa kama timu. Tunatanguliza malengo ya klabu kuliko mambo binafsi," alisema Goncalves.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, kiungo mshambuliaji Allan Okello amesema kwa mshikamano wa wachezaji wote, wanakwenda kupambana kama timu ili kupata matokeo mazuri katika mchezo huo.
"Kesho tunacheza dhidi ya timu yenye uzoefu mkubwa, yenye wachezaji wa kiwango cha juu na benchi lenye nguvu. Hivyo ni muhimu kwa sisi wachezaji kuwa na mshikamano na kupambana kwa dakika zote"
"Katika soka la leo kila timu ina wachezaji wazuri. Kinachofanya tofauti ni jinsi unavyotumia nafasi zako na jinsi unavyopunguza makosa. Tutahitaji umakini mkubwa, nidhamu na matumizi sahihi ya nafasi. Tunaheshimu wapinzani wetu lakini tunaamini pia katika uwezo wetu. Kila mechi ni fursa ya kuendelea kukua," alisema Okello



