Baada ya mapumziko ya wiki kadhaa kupisha michuano ya Afcon 2025 iliyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita na Senegal kuibuka mabingwa, michuano ya ngazi ya klabu ligi ya mabingwa (CAFCL) na kombe la Shirikisho (CAFCC) inarejea wikiendi hii.
Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya ligi ya mabingwa, Yanga wao wako ugenini leo kumenyana na Al Ahly, mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo.
Mtanange huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka barani Afrika, utapigwa saa 1 usiku katika uwanja wa Borg El Arab ulio mji wa Alexandria, Misri.
Yanga iliwasili Misri usiku wa juzi ambapo vijana wa kocha Pedro Goncalves walipata siku mbili za kujiandaa na mchezo huo.
Mchezo mwingine utapigwa majira ya saa 3 usiku Mamelodi Sundowns wakiwakaribisha Al Hilal ya Sudan.
Siku ya Jumamosi wawakilishi wengine wa Tanzania (CAFCL) Simba watakuwa dimbani kule Tunis kumenyana na Esperance.
Hii ni mechi muhimu sana kwa Simba kuhakikisha haipotezi ili kuweka hai mipango ya kufuzu robo fainali.
Simba iliyo kundi D, ilianza kwa kusuasua ikipoteza mechi zote mbili za mwanzo, na sasa wanapaswa kuanza kukusanya alama.
Kwa upande wa kombe la Shirikisho (CAFCC), wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo klabu za Azam Fc na Singida Black Stars zitashuka dimbani siku ya Jumapili.
Azam Fc wako ugenini Kenya kumenyana na Nairobi United wakati Singida BS watakuwa dimba la New Amaan Complex kumenyana na Otoho.