Klabu ya Simba SC imeendelea kuimarisha kikosi chake baada ya kuthibitisha usajili wa kiungo mshambuliaji Anicet Oura, raia wa Ivory Coast, aliyekuwa akicheza soka la kulipwa nchini Finland.
Oura, mwenye umri wa miaka 26, amejiunga na Wekundu wa Msimbazi kama mchezaji huru kufuatia kumaliza mkataba wake na klabu ya IF Gnistan ya Finland, hatua inayompa Simba nyongeza muhimu kuelekea nusu ya pili ya msimu.
Nyota huyo anajulikana kwa uwezo wake wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani, akimudu winga wa kulia, winga wa kushoto pamoja na kiungo mshambuliaji namba 10, hali inayompa kocha Steve Barker chaguo pana katika kupanga kikosi chake.
Usajili wa Oura unaelezwa kuwa mapendekezo binafsi ya kocha Barker, ambaye aliwahi kufanya kazi na mchezaji huyo katika klabu ya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini kabla Oura hajahamia Finland.
Katika msimu wa 2023/24 akiwa Stellenbosch, Oura alionyesha kiwango kizuri baada ya kufunga mabao nane katika mechi 35 alizocheza kwenye mashindano yote, akijijengea jina kama mchezaji mwenye mchango mkubwa kwenye eneo la mwisho la ushambuliaji.
Ujio wa Oura unatarajiwa kuongeza ubunifu, kasi na ushindani ndani ya kikosi cha Simba, hasa katika kipindi ambacho klabu hiyo inapambana kwenye mashindano ya ndani na kimataifa.