Klabu ya Coastal Union iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa aliyekuwa straika wa TP Mazembe ya DR Congo, Thomas Ulimwengu baada ya mazungumzo ya pande mbili.
Ulimwengu amefungua milango na tayari kukitumikia kikosi cha Coastal Union kwa mkataba wa miezi sita hadi mwisho wa msimu huu.
Nyota huyo aliyechezea timu za Soccer Akademia, Moro United, FC Vasby United, AFC Eskilstuna zote za Sweden, hakuwa na klabu yoyote ya ushindani tangu mara ya mwisho alipoachana na kikosi cha Fountain Gate, Julai 1, 2024.
Ulimwengu aliyecheza pia, TP Mazembe ya DR Congo, FK Sloboda Tuzla ya Bosnia and Herzegovina, Al-Hilal Omdurman ya Sudan na JS Saoura ya Algeria, ni pendekezo la Kocha wa Coastal Union, Mohamed Muya, anayetaka asajiliwe ili kuongeza nguvu.
Timu hiyo tayari imekamilisha usajili wa wachezaji watatu kipindi hiki cha dirisha dogo ambao ni Shiza Kichuya aliyecheza Simba na Namungo kisha msimu huu kuachana na JKT Tanzania, huku mwingine ni mshambuliaji, Abdulkarim Segeja aliyeondoka Tanzania Prisons. Nyota mwingine aliyejiunga na kikosi hicho ni mshambuliaji, James Msuva, ambaye hakuwa na timu pia.



