Mwamuzi wa mechi ya fainali AFCON 2025 kati ya Morocco dhidi ya Senegal Jean Jacques Ndala, hajapatikana na hatia baada ya uchunguzi kufanywa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Baada ya uhakiki wa kina, CAF imethibitisha kuwa hakuna makosa yoyote ya uamuzi yaliyotokea katika mechi hiyo yanayomhusisha mwamuzi huyo kutoka DR Congo.
Morocco iliwasilisha malalamiko CAF wakimtuhumu mwamuzi huyo kuwa hakuwatendea haki katika mchezo huo pale aliposubiri kuchukua hatua baada ya wachezaji wa Senegal kugomea kuendelea na mchezo.
Baadae Senegal walirejea uwanjani na Ndala akaruhusu mkwaju wa penati ambapo Morocco walikosa na kulazimu mchezo kwenda muda wa nyongeza.
Senegal wakafunga bao la ushindi katika muda huo ambalo lilitosha kuwathibitisha kuwa mabingwa wa Afcon 2025.
Morocco walitarajia mwamuzi huyo angemaliza mchezo na wao kutwaa taji la Afcon pale Senegal walipogomea mchezo.



