Mkufunzi wa Yanga Pedro Goncalves amesema maandalizi kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Al Ahly yamekamilika kikosi chake kikiwa tayari kukabiliana na mabingwa hao wa kihistoria Afrika.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, Goncalves amesema wanakwenda kwenye mchezo huo kwa tahadhari kubwa huku dhamira yao ikiwa kuibuka na ushindi.
Goncalves amesema Al Ahly wana wachezaji wengi wenye ubora na uzoefu mkubwa, wanaweza kukuadhibu kwa kila kosa utakalofanya.
Amesema wamejiandaa kwenda kukabiliana nao huku wakiweka mkazo kwenye umakini wanapokuwa na mpira na hata bila ya mpira.
"Tunaamini tunaenda kukutana na timu ambayo ipo bora ikiwa na mpira na isipokuwa na mpira na sisi tunapaswa kuwa bora tukiwa na mpira na tusipokuwa na mpira"
"Tulicheza vyema kwenye mchezo wa kwanza lakini tulifanya makosa ambayo wapinzani wetu waliyatumia kutuadhibu, tumefanya maborehso muhimu naamini tutakuwa na mechi nzuri hapo kesho"
Akiwazungumzia Al Ahly, Goncalves amesema kukosekana kwa kiungo Emam Ashour ni pigo kwao lakini upande wa kikosi chake hilo sio jambo la kulifurahia kwa sababu Al Ahly wana wachezaji wengi wanaoweza kutumika nafasi ya Ashour.
"Wao kumkosa Emam Ashour ni pigo kwao lakini kwetu hatuwezi kusema ni faida moja kwa moj. Zizo huwa anacheza sana pale kwenye timu ya Taifa na hata alipoumia Emam yeye ndiye alicheza. Ni lazima tujiangalie sisi wenyewe kwanza, wale wana watu wenye uwezo mkubwa," aliongeza Goncalves