Klabu ya Simba SC inakabiliwa na mtihani mzito wa kufa au kupona itakapokutana na Esperance Tunis siku ya Jumapili katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi inayotajwa kuwa ya maamuzi kwa hatma ya Wekundu wa Msimbazi katika kuisaka tiketi ya robo fainali ya michuano hiyo.
Mchezo huo unabeba uzito mkubwa siyo kwa kuwania pointi pekee, bali pia kwa kurejesha morali ya kikosi ambacho kimeanza mashindano hayo kwa matokeo yasiyoridhisha. Ndani ya Simba, kuna hali ya utayari na msisitizo mkubwa wa kuonyesha mshikamano na kupambana ili kubadili taswira ya timu kwenye hatua ya makundi.
Kocha Mkuu wa Simba Steve Barker amesema mchezo huo ni muhimu kwa timu nzima, akibainisha kuwa matokeo chanya yanaweza kuwa mwanzo wa kurekebisha makosa ya awali na kuijenga upya imani ya wachezaji pamoja na mashabiki.
"Ni kweli kwamba tumekutana na changamoto katika mechi zetu tatu za kwanza katika mashindano haya ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini huo sio mwisho wa safari yetu, bado tuna nafasi ya kufanya kitu katika mechi ambazo zimesalia."
"Mechi dhidi ya Esperance ni muhimu sana kwetu, sio tu kwa sababu ya pointi, bali pia kwa morali ya kikosi chetu. Tunahitaji kuonyesha msimamo wetu kama timu. Tukipata matokeo chanya, inaweza kuwa mwanzo wa kurekebisha kilichotokea. Hii ni mechi ambayo tunahitaji sana, sapoti ya mashabiki wetu," alisema Barker
Msimamo wa Kundi D, Stade Malien ya Mali inaongoza kwa pointi saba, ikifuatiwa na Esperance Tunis yenye pointi tano, huku Petro Atletico ikishika nafasi ya tatu kwa pointi nne. Simba SC ipo mkiani mwa kundi hilo ikiwa bado haijapata pointi hata moja.
Hadi sasa, Simba imekuwa timu pekee katika kundi hilo kushindwa kuvuna pointi. Ilianza kwa kupoteza nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Petro Atletico, ikafuata kipigo cha mabao 2-1 ugenini dhidi ya Stade Malien, kabla ya kupoteza tena kwa bao 1-0 dhidi ya Esperance.
Matokeo hayo yameifanya mechi ijayo dhidi ya Esperance kuwa ya lazima kushinda ili kufufua matumaini ya kusonga mbele. Simba inawahitaji mashabiki wake kwa wingi siku ya Jumapili kwani wao ni nguzo muhimu katika kuisukuma timu kupata matokeo chanya.



