Yanga inatarajiwa kurejea leo kutoka Morocco baada ya mchezo wa raundi ya tano ligi ya mabingwa kundi B wakikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa AS FAR.
Baada ya kurejea, hakutakuwa na muda wa kupoteza kwani vijana wa kocha Pedro Goncalves wanapaswa kuanza maandalizi ya mchezo wa maamuzi dhidi ya JS Kabylie ambao utapigwa Jumapili, Februari 15.
Kimahesabu Yanga bado ina nafasi ya kufuzu robo fainali, pamoja na kuwa watategemea matokeo ya mchezo kati ya Al Ahly dhidi ya AS FAR.
Ushindi kwa Al Ahly utafungua milango kwa Yanga kufuzu lakini Wananchi watahitaji kushinda kuanzia mabao mawili au zaidi ili kunufaika.
Kazi kubwa ambayo kocha Goncalves atahitaji kuifanya katika siku chache zilizobaki ni kuimarisha safu yake ya ushambuliaji hasa kwenye matumizi ya nafasi.
Katika mchezo dhidi ya AS FAR, kulikuwa na uwezekano wa Yanga kufunga zaidi ya mabao mawili kama washambuliaji wangetumia nafasi kwa usahihi.
Katika mchezo ujao hakutakuwa na lugha nyingine kama Yanga itakosa ushindi, hata kama AS FAR watapoteza dhidi ya Al Ahly watafuzu.
JS Kabylie hawatakuwa na cha kupoteza katika mchezo huo kwani tayari wamepoteza matumaini ya kusonga mbele hivyo hawatarajiwi kuja na mpango wa 'kupaki basi'.
Unatarajiwa kuwa mchezo wa wazi ambao pengine nafasi nyingi zitatengenezwa kwa kila upande.